Wednesday, September 8, 2010

Nafasi ya Lugha katika Elimu na Maendeleo ya Nchi

MTOTO anapoona vitu au kusikia mambo fulani kisha akafundishwa kitu au sauti hiyo inaitwaje au inatolewa na nini inakuwa ni rahisi kwake kuoanisha alichokiona au kusikia na dhana mpya anayojifunza.

Hii pengine ndio sababu kwamba nchi kama Urussi, China, nchi za Uarabuni, Korea, Japani, Malaysia, Indonesia zinafanya uzuri kiuchumi kwa sababu elimu na mafunzo yanatolewa katika lugha ambayo wananchi wake wanaielewa kwa kuwa wanaitumia kila siku.

Urahisi huu wa kujifunza unatokana na ule ukweli kwamba anayesoma kwa lugha yake mwenyewe anakuwa na kazi moja tu. Kazi hiyo ni kuelewa maudhui ya somo husika vizruri iwezekanavyo. Wakati yule anayesoma kwa lugha ya kigeni hulazimika kwanza kujua maana ya maneno na dhana katika lugha nyingine kabla hajaanza kupambana kujua maana ya somo lenyewe.

Kusoma katika lugha ya nyumbani ni sawa na kusoma na kujifunza kwa vitendo wakati ambapo kusoma kwa lugha ya kigeni ni sawa sawa na kufundishwa nadharia tu bila vitendo ndani au nje ya darasa.
Hii ni dhahiri kuwa njia ya kwanza itamsaidia sana mwanafunzi kuelewa na kuhifadhi mambo mengi zaidi kwa faida ya baadaye kuliko njia ya pili. Ambayo kwa jinsi inavyoendelea kuacha kutumika kwa mapana na marefu bali mtumiaji wake anasahau dhana nyingi alizojifunza kwa lugha hiyo.

Elimu na ujuzi sio kusoma vitabu kwa wingi na kuhudhuria mihadhara bali ni kile kiwango cha vitu unavyovikumbuka mara baada ya kumaliza shule. Kwa mantiki hii Watanzania wengi wamesoma lakini hawajaelimika maana elimu yao haiwasaidii sana katika kutatua matatizo yao ya kimaisha,kijamii na kiuchumi.

Lengo kubwa la elimu ni mawasiliano. Na mawasiliano yanakuwa na maana pale wanaowasiliana wanaelewana vizuri kabisa na kwa haraka zaidi kuliko kinyume cha hivyo.

Tatizo kubwa linaloisibu nchi yetu ni kuendelea kung'ang'ania watoto wetu kufundishwa katika lugha za kigeni (zinazotoka kwenye nchi zinazodidimia kiuchumi) badala ya watoto wetu kufundishwa kwa lugha yetu wenyewe au angalau lugha ya zile nchi ambazo sasa zinapaa kiuchumi.

Ingawa Tanzania ilishakubali kutumika kwa lugha ya Kiswahili katika shule za msingi imekuwa ni mwendo wa mbele nyuma katika kufikia uamuzi wa kuitumia lugha hiyo kufundishia sekondari na vyuo vikuu.

Baya zaidi ni kuwa pamoja na kuwa na watu ambao wako tayari kuanzisha sekondari na vyuo vikuu vinavyotumia Kiswahili, Kiarabu na lugha nyingine zaidi ya Kiingereza watu na taasisi kama hizo wamekuwa wakipata wakati mgumu katika kufanikisha azma yao hiyo.

Serikali yenyewe kwa kutingiwa na matatizo yaliyopo sasa hivi katika sekta ya elimu imekosa nafasi na rasilimali zinazohitajika ili kuendesha tafiti za ufundishaji kamilifu ambazo zingelichangia kwa kiasi kikubwa kufikia maamuzi juu ya lugha ya ufundishaji mashuleni na vyuoni.

Jambo jingine kubwa la kuifanya jamii inufaike na elimu na ujuzi unaojengeka katika jamii mwaka hadi mwaka ni lile la kuwa na utafiti na uvumbuzi endelevu katika kila eneo la kijamii na kiuchumi.

Utafiti na uvumbuzi ndio vitu vikubwa vinavyotofautisha kati ya nchi zinazopiga maktaimu na kutokuendelea na hatua zinazosonga mbele na kuendelea kila mwaka, kila muongo, kila karne.

Tanzania haitafanikiwa kuanza kuelekea kwenye maendeleo mapana, ya kina, yenye uvumbuzi na uendelevu na ya kudumu iwapo uamuzi wa kutumia lugha ya Kiswahili kufundishia hautafanywa mapema kadri iwezekanavyo. Na kuna wanaothubutu kusema kwamba shujaa wa kweli Tanzania atakuwa ni yule kiongozi ambaye atafanya maamuzi sahihi kuhusiana na lugha ipi itumike katika kuijenga na kuiendeleza Tanzania ya karne ijayo.

Wakati bado tunasubiri uamuzi huo wa kutumia lugha ya Kiswahili kufundishia sekondari na vyuo vikuu angalau katika shule maalum za majaribio (zitakazotumia lugha mbili au tatu kufundishia ikiwemo Kiswahili) ni muhimu kwa wakati huu kuamua kuwapatia Watanzania waliomo na wasiomo mashuleni-masomo muhimu ya kimaendeleo katika lugha ya Kiswahili. Masomo hayo ni pamoja na Menejimenti au Utawala; Menejimenti ya Rasilimali watu; Menejimenti ya Fedha; Menejimenti ya Masoko au Nunuauza; Uchumi; Nadharia za Uongozi; Tabia za Taasisi au Oganaizesheni; Saikolojia na Sosholojia katika Menejimenti na mengineyo kama hayo.

Hili linatulazimisha kuanza kufikiria uwezekano wa kuunda majopo ya wataalamu mbalimbali kuandaa kamusi la kila somo tayari kwa kazi ya kuifanya lugha hii itumike kwa mapana na marefu zaidi.