HAKUNA Chama chochote cha kisiasa nchini hivi leo au kesho kinachoweza kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Watanzania. Wanaoweza kufanya hivyo ni wananchi kwa umoja wao na katika makundi yao ya kijamii kwenye mtaa, kata, wilaya na mikoa.
Kwa kutambua hili serikali za Tanzania zote baada ya awamu ya kwanza (chini ya chama kimoja) zimegeuka abautani na kukaribisha kwa mikono miwili ujinga, umaskini na maradhi kama njia pekee ya kuhakikisha Chama Tawala kinaendelea kuwa madarakani.
Si kweli kuwa wanasiasa wanaweza wakakubali ujinga uondoke vijijini. Kufanya hivyo ni kuruhusu upinzani kuteka maeneo hayo kama walivyoteka maeneo kadhaa ya mijini.
Rushwa inayotolewa na viongozi vijijini ukichanganya na ujinga na uoga mkubwa wa mabadiliko katika maeneo hayo kunawafanya wanavijiji kile kilicho bora katika kubadili maisha yao-yaani, neema na mapinduzi ya kweli yanayoletwa na demokrasia na mfumo wa vyama vingi.
Kwa kutmbua fika ukweli huu, wanasiasa wa vyama tawala barani Afrika wamedhamiria kuona ujinga unaendelea kuwepo barani humu ili wanufaike na faida zinazoletwa na ujinga huo.
Anayekwambia kwamba kuna kiongozi yeyote wa Afrika anayetaka umasikini utoweke Afrika ni mwongo. Hakuna kiongozi hata mmoja Afrika anayetaka umaskini uondoke.
Umaskini ukiondoka kwanza viongozi hao watakosa fedha za misaada zinazowatajirisha. Pili, wananchi wasiokuwa maskini hawawezi wakayumbishwa na hongo ya kanga, vitenge na pilau.
Na tatu, umasikini ndio unaojenga watu kutokujiamini, ufukara ukitoweka Tanzania basi Watanzania wengi watajiamini na hivyo kuwa huru zaidi kuchagua kile wanachokitaka na sio vinginevyo.
Aidha, kwa kuacha kuitumia kodi ya wananchi ili huduma za tiba na afya zitolewe kiubinadamu na bila upendeleo kwa aliye nacho na asiye nacho serikali yetu kwa makusudi imewageuza wananchi kuwa watu wasio na uhakika na kesho yao.
Vilevile, kwa kuwaonesha wazungu na wageni wengine kuwa wao, yaani, viongozi wetu wa serikali, wanaamini kwamba watu wetu madini yetu na rasilimali zetu nyingine hazina thamani kama wao, mitaji na mitambo yao -watu wetu wamedunishwa na kuwekwa katika udhalili wa muda mrefu na pengine mpaka mwisho wa dunia. Katika hali kama hii, ambayo inakwenda pamoja na kugeuza nchi yetu kuwa jalala la kuuziwa bidhaa duni na za ovyo toka kila pembe duniani basi watu wetu ni muhali kujiamini na kujiingiza katika ushindani wowote wa maana katika dunia hii. Isitoshe, kwa kudharau kuitumia lugha yetu yenyewe na kuendelea kutumia lugha ya kigeni bila nchi hii kuwa na siri wala fikra zake za asili na fasili basi uwezekano wa nchi hii kuja kuzinduka chini ya uongozi wa wanasiasa waliopo hivi leo sio kitu cha kuyumkinika.
Umma hauwezi ukawa unapenda hili au lile, lakini wanasiasa au chama fulani likalazimisha vinginevyo. Kinachohatarisha amani na utulivu katika maeneo mengi ya nchi yetu leo ni kwa wanasiasa fulani kutumia nguvu za dola vibaya, kuikwaza demokrasia na wao kuwaamuliwa wananchi na kuwanyima kile wanachokitaka na kuwapa kile wasichokitaka.
Katika mfumo ambao Chama Tawala kinaweza kuchagua hata watu wenye matatizo kuwa maofisa wakuu serikalini, mabalozi, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakuu wa benki, wakuu wa mashirika mbalimbali ni dhahiri kwa hapa ndani kwamba maendeleo ya kila mkoa na wilaya yatategemea uwezo au kutokuwa na uwezo wa mkuu anayesimamia husika.
Aghalabu wale wasio na uwezo na ambao wameupata ukuu huo kwa bahati nasibu, huwa ni kombakomba wa kubwa katika kujipendekeza kwa viongozi wakuu. Wakati mwingine hudiriki hata kuvunja haki za binadamu ili kuonesha utii na uaminifu wao kwa kiongozi wa nchi na watu kama hao.
Ni lazima wananchi wetu waeleweshwe kwa kituo kwamba viongozi ni watu kama wao. Na kwa sababu ni binadamu viongozi hao wanaweza wakawa wacha Mungu au wauaji; wanaweza wakawa watu wema au watu wabaya; wanaweza wakawa wezi au watu waaminifu; wanaweza wakawa wakweli au waongo; wanaweza wakawa viumbe wenye utu na ubinadamu au kinyume cha hivyo.
Ili nguvu ya umma ianze kufanya kazi ni wajibu na jukumu la kila mmoja wetu aliyefunguka macho na baada ya kutambua nchi hii ilikotoka na inakotakiwa kwenda kukaa mpango wa kuhakikisha kuwa nchi inakwenda kule tunakotaka iende na sio kule viongozi wachache waliopotea na wasio na uzalendo wa kweli na wa dhati wanakotaka kutupeleka.
Bila kujali sisi ni kabila gani, dini gani, hali gani, jinsia gani na kadhalika tuungane kama kitu kimoja kwanza kwa kubainisha dhahiri ni nini visheni ya kule tunakotaka kwenda. Tunataka tufanikishe mambo gani wakati wa uhai wetu. Tusikurupuke kama wenzetu walivyozoea kukurupuka kila siku na kufanya kazi kizimamoto. Majukumu na wajibu tutakobeba lazima utokane na maamuzi na mipango mizuri ambayo imedhamiriwa kuwepo ili kufanikisha azma zetu za kuwa watu na taifa bora. Maamuzi na mipango inayokataa katakata mtu mmoja au kikundi cha watu wachache kujifanyia mambo jinsi apendavyo bila kufuata katiba, miongozo na sheria tutakazojiwekea.
Lazima wananchi waweze kujipanga kama vile wao ni serikali mbadala kando ya serikali iliyopo ili tuweze kuelimika, kupata maarifa na kujua kile tunachotakiwa kukifanya na kukidhibiti kama tutakavyotakiwa kujua viongozi wetu na watumishi wa serikali zetu wanachotakiwa kukitekeleza, kwa gharama gani, rasilimali gani, ubor aupi na kwa wakati gani.
Kuifupisha kazi hii nitaorodhesha maeneo machache tu ambayo 'Nguvu ya Umma' inaweza ikaanza kuonesha umuhimu, utakikano na sababu ya kuwepo kwake na kuonekana sio tu ipo bali inafanya kazi.
Suala la Katiba. Nchi yetu ina Wanasheria, viongozi wa dini, wanasiasa na mabingwa wa fani mbalimbali wanaoweza kuketi pamoja na kututengenezea katiba mpya.
Kinachoonekana sasa hivi ni kuwa chama tawala kimegawanyika kati ya wataka viraka na wataka katiba mpya. Wataka katiba mpya, kwa kutambua kuna maslahi katika kusimamia kuundwa kwa kariba mpya wanataka kuteka nyara madai ya kuwa na katiba mpya. Wanaelewa fika wakikubali kuwepo kwa katiba mpya basi misaada yote ya ndani na nje itadhibitiwa nao. Na juu ya yote watakuwa katika nafasi bora zaidi ya kutengeneza katiba ambayo itakuwa inawapendelea wao na chama chao.
Wataka viraka, wanafanya hivyo ili kulinda maslahi yao, nafasi zao za kazi au maslahi na mustakabali wa familia na watoto wao.
Ni dhahiri wanaopaswa kusimamia mabadiliko ya katiba hawastahili kutoka kwenye kundi lolote kati ya haya. Ni muhimu waunda katiba mpya wakawa ni Watanzania wasiopendelea chama au kundi lolote la watu hapa nchini.
Mikoa huru kiuchumi na kijamii. Ipo habari eti Zanzibar itakuwa mkoa, huko ni kuturudisha nyuma. Kinachostahili kutokea ni kwa kila mkoa kuwa kama Zanzibar. Ila badala ya mkanganyo wa Urais pakawa na waziri mkuu wa mkoa na baraza lake la mawaziri. Mikoa ikiwa na baraza lake la mawaziri sio rahisi kwa wanasiasa uchwara na wasiokwenda shule kuja madarakani kama inavyotokea sasa kwa wanasiasa wa chama fulani nchini.
Eneo moja la nchi eti kuwa na rais na mawaziri wanaopigiwa kura na watu wasiofikia hata laki tatu na nusu, lakini kupata mameya na madiwani halali na safi tu katika mikoa yetu, bila kuzungumzia kuwa na mkuu wa mkoa anayechaguliwa na wakazi wa mkoa husika na baraza lake la mawaziri ni mkanganyiko mkuu wa kimfumo na haki ya kikatiba kwa wananchi kujiamulia mambo yao wenyewe.
Misaada na Wafadhili. Ni muhimu Watanzania wenye fani za menejimenti, uchumi na fedha kutusaidia kujua na kupromoti aina ya ufadhili na misaada itakayotutoa toka kwenye umaskini badala ya kuendelea kukaribisha misaada inayotupa samaki kila siku badala ya kutupa nyavu sisi wenyewe tukavue baharini, mitoni au maziwani.
Umeme. Watanzania tukingoja mpaka serikali iwe na akili ya kutupatia umeme wa uhakika tutajikuta tunachina si baada ya muda mrefu. Lazima mabingwa wa uhandisi na hususan fani ya umeme na uzalishaji nishati wachukue hatua za kwanza kuanza kutukomboa. Nina hakika wakiketi katika simposia watakuja na mambo mengi ikiwa pia njia mbadala za uzalishaji umeme na hivyo kurahisisha nchi nzima kupata umeme kuliko muda uliopangwa na serikali.
Maji na Umwagiliaji Maji. Huko Moshi kijiji cha KIkavu Chini hakina maji kwa miaka miwili sasa. Wananchi wake maisha na uhai wao ulitegemea kilimo cha umwagiliaji. Hata hivyo, hivi leo hawana maji na ghafla wamejikuta ni watu fukara. Makundi ya kijamii ni muhimu kuzuia jambo kama hili lisitokee. Wakuu wa serikali wanaolipwa mshahara kila mwezi hawana uchungu na hili, na wanasiasa wanaongojea tena kuchaguliwa baada ya miaka mitano hawana habari kabisa.
Maji ni tatizo kubwa zaidi ya vile viongozi wetu wanavyodhania. Haiwezekani wao wenyewe kuwa na majibu ya kutosha katika hili. Ipo haja ya kuongeza kasi ya uanzishwaji wa miradi ya kijamii ili kutunusuru na ukosefu mkubwa wa maji katika sehemu mbalimbali za nchi katika miaka inayokuja.
Shule na Vyuo Binafsi. Hivi sasa kila mtu anajua fika kwamba shule na vyuo binafsi vinatuibia Watanzania kushoto na kulia. Chukulia mfano wa ada ya kati ya milioni 1.5 hadi 2.5 inayolipwa kwa baadhi ya shule ya msingi na kisha mtoto kila muhula kwa mihula mitatu anatakwa awasilishe bunda la karatasi (rim of paper) ambalo moja hugharimu zaidi ya shilingi 10,000. Kwa maneno mengine, ikiwa shule ina watoto elfu moja mwenye shule na walimu wake fumba na kufumbua wanapata shilingi milioni 10 za bure. Hili linafanywa na shule ndogo kwa kubwa ikiwemo zile za watukufu wabunge wetu.
Kama ilivyo kawaida ya wanasiasa wetu na serikali yao-pamoja na kusikia kilio hiki cha wazazi, kwa kuwa baadhi ya wamiliki wa shule hizo wanakisaidia chama tawala, uamuzi juu ya kuundwa kwa chombo cha kuratibu ada na gharama nyingine za shule hauwezi kufanyika haraka.
Uchimbaji Madini. Wapo wenye mawazo kwamba Tanzania iwatumie wataalamu wake wa madini waliosomeshwa ndani na nje, ili mradi walipwe kama wazungu wanavyowalipa wanaowaajiri kutoka kwao na ndani ya nchi, washawishike kufanya kazi kama waliopandwa na pepo. Tukope, tuwe na mitambo yetu wenyewe lakini madini tuyachimbe sisi wenyewe na sio vinginevyo.
Hili halihitaji mchango wa serikali. Matajiri na taasisi za Kijamii zikijipanga uzuri na kwa kushirikiana na wachimbaji toka China, Malaysia, Korea, Uarabuni ambao sio waroho kama hawa waliopo tunaweza kabisa kuhakikisha utajiri wetu wa asili unakuwa utajiri unaowafaa wananchi wetu wenyewe hapa nyumbani badala ya kwenda kuwanufaisha wageni huko nje.
Ajira kwa Vijana. Vijana wengi wa Kitanzania hawana ajira. Je, tukae na kuisubiri serikali ije na miujiza? Au kuna wenye uchungu na nchi hii wanaoweza kuanzisha vuguvugu la kijamii likahakikisha kuwa hili linafanyika.
Nimewahi kuzungumzia juu ya uwezekano wa nyumba kwa kila familia Tanzania. Hebu tuliangalie kwa undani zaidi hapa. Ninachosema mimi hapa ni kuwa ujenzi huo wa nyumba kwa kila familia ni programu ya kipato ambayo inaweza kufadhiliwa na wananchi na wale wanaotakia wananchi wa Tanzania mema na sio lazima serikali.
Kinachotakiwa kufanyika ni kupata fedha ya mbegu ili kuwawezesha vijana wa mkoa au mikoa fulani kuzalisha matofali yote yanayohitajika; kisha wale wa mikoa mingine kupewa jukumu la kutengeneza vigae au vifaa vinavyofaa kuezekea; na kisha wengine wakapewa kazi ya kutengeneza milango na madirisha na vifaa vya ndani. Kwa namna hii, vijana wa kila mkoa watalipwa kwa kazi yao na kisha wanachozalisha kitakwenda kutumika katika ujenzi wa nyumba katika kila mkoa na baada ya miaka 10 mradi huu utakuwa umewanufaisha watu na kuingiza biashara na ajira mpya badala na hivyo kututoa kwenye ngazi moja ya maendeleo na kutupeleka kwenye ngazi ya juu zaidi.
Ni wazi mpango huu ukifanikiwa, nchi nyingi za Kiafrika zitahitaji watu wetu kwenda kwao kuigilizia jambo hili. Neema iliyoje? Swali ni Je, wanasiasa wanaliona hili ?
Nimetoa mifano michache. Hoja yangu i wazi. Watanzania tukidhamiria tunaweza kuondosha umasikini kabisa na kufanya chochote tunachokitaka. Lakini lazima tuepukane kwanza na wajanja ambao wanadhani wanaweza kuendelea kuiibia nchi, BOT, Hazina na wizara zetu mwaka nenda mwaka rudi na nchi ikanusurika na uovu wao. Lazima serkali iwe ya chama ambacho wizi na rushwa kwake ni haramu ndio tu tutaanza kuelekea kwenye njia ya kweli ya kuupiga vita umasikini na kukosa maendeleo.
Ni vigumu kuwazia maendeleo chini ya utawala wenye chuki, uonevu, dharau, dhuluma, wizi, upendaji ukubwa na makubwa bila kuyatolea jasho na wanasiasa wanaoiingiza nchi katika madeni makubwa makubwa na ya ajabu kila mwaka -ambayo yote ni wiiiiiiziiiii mtuuuupu!!!
Watanzania lazima wajipange na kusema waziwazi: 'Hakipendwi chama hapa bwana, tunataka maendeleo. Ubaguzi wa kichama lazima ufe. Na viongozi wawe ni watu walochaguliwa, wanaofaa na wanaoweza kuifanya kazi mbele yao na sio eti tu kwa sababu ni wanachama wa chama fulani. Mathalni, mikoa ya Arusha, Mara na Kigoma kwa hali yoyote ile ilistahili kuwa na uongozi wa Vyama vya upinzani. Pengine hata mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya wakitoka upinzani.' Haya yanawezekana kwa kukataa mifumo iliyopo kupitia katiba mpya itakayoondoa mapungufu yote yaliyoko katika katiba ya sasa.
Contributions to People who Matter!
No comments:
Post a Comment