NINAAMINI kwamba kila familia ya Kitanzania inastahili, ina haki na inaweza ikawa na nyumba bora ya angalau vyumba viwili kwa kuanzia.
Lakini siamini hili linaweza kufanyika kwa kushusha bei ya vifaa vya ujenzi peke yake bali pia kwa mikakati maalum yenye msukumo toka serikalini, mabenki na wahisani wengine wanaotaka kuufuta kabisa umaskini wa kupindukia hapa nchini.
Ndoto hii inaweza ikatimia sio kwa kuwapa watu nyumba bure bali kwa wao wenyewe kutoa mchango wa aina moja au nyingine katika kufanikisha hili. Aidha, kama tunavyofahamu sekta ya ujenzi hutoa ajira nyingi kwa vijana. Dhamira ya kuipatia kila familia nyumba bora hapa nchini itakwanda mbali sana katika kuwapa ajira vijana kwenye mikoa mbalimbali na wakati huo huo kuwawezesha na wao pia kuwa ni wamiliki wa nyumba.
Stori za saiti na watu kujenga nyumba kila uendako zitakuwa ni stori zilizopitwa na wakati kwani sasa watu watakuwa wanashughulika na yale yanayoongezea utajiri nchi na sio tu ujenzi wa nyumba.
Kwa maneno mengine, jambo linaloonekana kuwa leo ni tatizo, yaani, wananchi kukosa nyumba bora, kwa kutumia ushauri huu, fumba na kufumbua litageuka kuwa ni fursa ya ajira kwa mamilioni ya vijana nchini; ujenzi wa nyumba bora na ubadilishaji wa makazi na mandhari ya nchi toka ile ya shida na umasikini kwenda kwenye ile inayoonesha kwamba angalau watu wetu wanasetirika na wanaishi kwenye nyumba ambazo hawatasita kumkaribisha mgeni.
Katika matangazo yanayonikera sana hapa nchini ni pamoja na lile ambalo linaonekana kushangiliaumasikini wa wananchi vijijini kwa kuonesha nyumba ya udongo iliyoezekwa kwa majani.
Na eti wanaoishi humo wana afya na wanawiri kwa sababu wanatumia chandarua kilichotiwa dawa !
Tangazo hilo linahusiana na matumzi ya neti kupinga malaria. Halinikeri kwa kuwa lina uongo zaidi ya ukweli kwa kuwa malaria haiwezi kutoweka kwa kutumia neti tu, lakini zaidi ni ile hali ya kuonesha kuwa vyandarua vilivyotiwa dawa ni bora kuliko nyumba kwa wananchi vijijini. Hili limenishinda kumeza. Na ninalitema kama lilivyo.
Kama kuna zawadi ya mwaka mpya ambayo ningelipenda Watanzania wenzangu wanaoishi katika manyatta, tembe, msonge na kadhalika wapate ni ile ya uhakika kuwa nchi sasa imedhamiria kila familia iwe na nyumba bora kwa kutumia vifaa, nguvu-kazi, na rasilimali zetu wenyewe papa hapa nchini
Usanii au utangazaji unaosherehekea na kutukuza alama za umasikini wetu, ninaamini, zinaweza kuwa ni kikwazo katika kumwelewesha mwananchi kuwa hali aliyo nayo sasa haikubaliki na hakuhumiwa wala kuumbwa katika dhiki na uhitaji.
Baada ya kubaini kuwa Tanzania haina fedha, Baba wa Taifa, Mwalimu J. K. Nyerere hata hivyo aligundua kuwa akili na nguvu za Watanzania zikielekezwa katika kuboresha maisha yao kwa njia mbalimbali ni sawa na fedha au mtaji wenye thamani wakati mwingine sawa na ule wa pauni au dola za nje.
Kwa maneno mengine, Nyerere kama mwanasaikolojia alijua kuna matumaini au matarajio katika mioyo ya watu wake; kisha kwa kutumia kipaji cha kuzungumza na watu wa hali zote akaweza kuwaunganisha Watanzania kiasi cha kuwa na ndoto moja ya maendeleo na ustawi; na kisha kwa kutambua hatuna fedha, akaamua akili na nguvu za wananchi wake ndizo mtaji muhimu kuliko wote endapo nchi hii kweli inataka iondokane na umaskini. Ili mradi akili na nguvu hizo hazitumiki kuwanufaisha na kuwatajirisha watu wachache tu miongoni mwetu.
Kwa bahati baada ya kuondoka yeye utawalani viongozi waliofuatia aidha wamesahau kabisa juu ya rasilimali hii au wameufanyia usanii kama vile kuita 'mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe' lakini mtaji huu haujaelekezwa katika kuleta mabadiliko ya kimaisha tunayoyataka yawepo hapa nchini.
Fursa kwa wananchi kutumia nguvu na akili zao kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa bado zipo. Tofauti tu na miradi ya kupunguza umaskini iliyopo hivi sasa jambo linalotakiwa ni kuwa na miradi ambayo fedha zote zinakwenda kwa maskini wenyewe moja kwa moja kwa njia ya mishahara na malipo ya bidhaa au kazi mbalimbali watakazozifanya. Kwa maneno mengine, fedha na misaada ya kuwaondoa masikini kutoka kwenye umasikini zisitumike kuwatajirisha wanasiasa, maofisa wa serikali na maofisa wa mashirika yasiyo ya kiserikali.
Ujamaa na Kujitegemea unaweza usihitajike katika maeneo mengine, lakini katika hili la lujenzi wa nyumba na makazi bora ya watu bado sera hiyo ni muhimu kama ikitazamwa na kupangwa upya kwa manufaa ya wananchi wenyewe na sio walanguzi wa kisiasa na kiserikali.
Hata hivyo, ni dhahiri kuwa kwa wasiojua na wasioelewa kinachoendelea katika nchi yetu sio rahisi mpango au programu ya kuondoa kiukweli umaskini kukubalika hapa nchini.
Binafsi ninaamini kwamba kuwezesha kila familia nchini kuwa na nyumba bora ya hata vyumba viwili ndio njia bora zaidi ya kupambana na umaskini kuliko yoyote iliyopo hivi leo.
Ila njia hii ni lazima itapigwa vita kwa sababu kadhaa. Kwanza, inamkomboa mwananchi nawanasiasa wadanganyifu wanaoendelea kuwa madarakani kutokana nawananchi kuwawajinga, wasio na afya bora na masikini wa kutupwa; inawapa wananchi uwezo na uhuru zaidi kijamii, kisiasa na kiuchumi; kitendo cha kushiriki katika ujenzi wa nyumba ya kwanza humpanua sana mtu akili na matazamio yake na inaleta ajira kwa jumuiya na kupunguza umaskini.
Ni njia ambayo pia huwawezesha wananchi wa kawaida kufunguka macho na wakatambua kwamba wanastahili kuwa wamilikaji wa nyumba na sio wapangaji tu; wanastahili kuwa nacho kama walio nacho walivyo na ndio njia sahihi zaidi ya kumtoa Mtanzania kwenye umaskini wa kutupwa na unaonuka hadi nje ya mipaka yetu.
Nyumba na Mkakati Dhidi ya Umasikini
Nchi yetu ina mikoa 30 hivi sasa. Pendekezo langu ni kuigawa mikoa hiyo katika mafungu matatu, yaani, kila kundi likiwa na mikoa 10.
Nyumba ina sehemu kubwa tatu. Sehemu hizo ni msingi na kuta; halalfu paa na dari na tatu, milango, madirisha na samani mbalimbali.
Kinachohitajika kufanyika ni kwa vijana wa mikoa kumi ya kwanza kushughulika na uzalishaji matofali, hususan yale ya kuchoma na yale ya mchanga. Au matofali ya kukatwa toka kwenye majabali laini. Matofali hayo yatanunuliwa na serikali kwa ajili ya usambazaji nchi nzima. Matofali hayo yatasambazwa kote nchini kwa ujenzi katika programu yetu ya Nyumba kwa kila familia.
Ndivyo itakavyokuwa pia kwa utengenezaji wa vigae au mabati au kifaa mbadala kitakachotumika kama paa katika mikoa kumi nayofuatwa. Vifaa hivi vitanunuliwa pia na serikali na kusambazwa kwa namna ambayo wote waliopo katika cheni ya uzalishaji, usafirishaji na matumizi yake utakuwa unaeneza pato zuri kwa wale wanaoshiriki katika kazi hii.
Mikoa inayofaa kutengeneza milango, madirisha na samani nayo itakuwa 10 na watakaoshiriki katika kazi hii nao watanufaika na pato la uhakika katika muda wote wa uhai wa programu ya Nyumba kwa Kila Familia.
Programu isiwazuie wakazi wanaopenda kuonesha utundu na ubunifu utakaotoa dizaini au sampuli mbalimbali za majengo au hata wale watakaoweza kujenga vyumba zaidi ya viwili kwa kutumia akili au ujanja zaidi. Kubwa hapa ni kwamba, ujenzi wa nyumba unapewa kipaumbele cha kwanza na kuwa akili, masikio na macho yetu yote yanaelekezwa huko. Wakati tukijenga matumaini kuwa mwisho wa ujenzi wa nyumba sote tutajipanga vizuri zaidi kutafuta maendeleo na mafanikio ya juu zaidi.
Ujenzi wa nyumba kwa kutumia akili na nguvu za wananchi wetu na msaada kidogo toka serikalini na wafadhili wa ndani na nje. ni jambo linalowezekana. Na hasa ikiwa BOT, Hazina, Kampuni za Simu za Mikononi, Peteroli na Mabenki na Wafadhili wengine wa ndani na nje ya nchi watahamasishwa kuwalipa ujira wa aina fulani wale watakaochangia katika uzalishaji wa vifaa mbalimbali vya ujenzi.
Kwa maneno mengine, endapo kila familia nchini itakuwa na nyumba bora biashara zote zina uwezo wa kukua mara mbili au tatu zaidi kuliko zinavyokuwa kwa hivi sasa.
Programu hii ninaiona ni nzuri kwa sababu fumba na kufumbua ikipata ushirikiano wa serikali inatoa ajira kwa maelfu kama sio mamilioni ya vijana. Kubwa zaidi itajenga imani ya hali ya juu kwa serikali na viongozi wake. Hapa sasa litaonekana angalau jambo moja ambalo serikali imemfanyia kila Mtanzania tofauti na hivi sasa.
Ya kuepuka hapa ni kutokujenga tena nyumba za pamoja karibu karibu sana. Utekelezaji wa mpango huu ni njia pia ya kuondokana na misongamano, foleni na hatari nyingine zinazokuwatishio katika maisha yetu ya kila siku. Nyumba ziwe na nafasi ya angalu nusu ekari kama sio ekari nzima.
No comments:
Post a Comment